19 Machi 2011 - 20:30

Maelfu ya Wamisri jana waliandamana katika mitaa ya Cairo mji mkuu wa Misri wakilalamikia hatua ya wanajeshi wa nchi hiyo ya kuwakandamiza wanawake na wasichana kwa kuwapiga na kuwadhalilisha katika maidani ya Tahrir.

Wanaharakati wa kike wa Misri waliitisha maaandamano hayo jana ili kupinga mashambulizi dhidi ya wanawake na kutaka kukomeshwa mara moja vitendo hivyo vya utumiaji mabavu dhidi ya waandamanaji. Maandamano hayo yamefanyika masaa machache baada ya vikosi vya usalama vya Misri kupambana na waandamanaji katika mji mkuu wa Misri katika siku ya tano ya mfululizo wa machafuko yaliyopelekea kuuawa raia 14 na kujeruhiwa wengine zaidi ya 900 tangu Ijumaa iliyopita. Wananchi wengi wa Misri wamelaani machafuko yaliyojiri katika maidani ya Tahrir khususan baada ya polisi wawili wa nchi hiyo kuonyeshwa katika picha wakimburuza chini mwanamke mmoja kwa kutumia blauzi yake, huku wakimkashifu kwa kuweka wazi nguo zake za ndani na baadae kumpiga kwa marungu na kumkanyaga mwilini. Wakati huohuo Jenerali Adel Emara mjumbe wa baraza la kijeshi linalotawala huko Misri amesema shambulizi lililofanywa dhidi ya mwanamke huyo ni tukio la kando na kwamba hivi sasa linachunguzwa.